KWAKO Agness Gerald ‘Masogange’ pamoja na wenzako wengi ambao baadhi yao nitawataja kwa majina hapo chini. Nawasalimu katika jina la Bwana, vipi mko poa? Mnajionaje na hali? Mishe zenu zinakwenda kama kawaida?
Mkitaka kujua afya yangu, mimi namshukuru Mungu. Naendelea vizuri. Nazidi kupambana ndani ya huu mjengo mkubwa wa Magazeti Pendwa Tanzania, Global Publishers Ltd. Kazi yetu ni ngumu kidogo, kila siku wasomaji wanataka habari mpya. Kuzitafuta si kazi ya kitoto.
Dhumuni la kukuandikia barua Masogange na wenzako leo ni moja tu, kutaka kuwakumbusha kwamba kuna maisha baada ya ujana. Umaarufu mnaoupata kwenye mitandao, hauna maana kama mnakuwa hamna shughuli ya kufanya.
Watanzania hawafurahishwi na mnavyoposti picha zenye viashiria vya ngono na kuziweka mtandaoni. Unajipiga picha ya nusu utupu, unaiweka mtandaoni ili iweje? Umekaa mkao wa kuhamasisha ngono unataka kutafsirika vipi? Unajiuza? Kama ndiyo biashara, kwa nini usitafute nyingine?
Mbona biashara zipo nyingi jamani. Kupitia urembo wenu mbona kuna ishu kibao tu za kutengeneza fedha? Kuna makampuni yanataka kufanya kazi na nyinyi kwenye matangazo yao, kuna wasanii wanataka muwapambie video zao, yote hayo hamyaoni? Njia pekee ya kuishi ni hiyo mliyoichagua?
Wiki iliyopita niliona moja kati ya habari iliyopamba magazeti ya Global ni ile ya mtindo mpya wa mastaa kujiuza. Kwamba siku hizi taarifa zinaeleza kwamba wengi wenu mnapoweka picha kwenye mtandao wa Instagram, mnapata dili nchi za nje.
Hii ni aibu. Kweli warembo wa Tanzania mmefika hapa? Yaani biashara inafanyika mtandaoni, mnasafiri kwenda nchi za watu kweli? Sikushtuka sana nilipoona ile habari maana Masogange wewe na wenzako mmekuwa mkisafiri pasipo kueleweka kinachowasafirisha.
Utasikia tu Masogange yupo Sauz, sijui Gigy Money yupo wapi mara sijui Kidoa alikwenda kufanya shopping Dubai na kurudi, mnakwenda kule kwa kipato gani? Kazi gani zinazowaingizia kipato hadi muende kule kufanya shopping?
Niliwahi kuzungumza na wewe Masogane siku moja katika Global TV Online. Nilikubana maswali kuhusu kazi inayokufanya uishi mjini, hukuwa na jibu la kueleweka. Bado pia ulisema wasanii hawawalipi vizuri pindi mnapotumika katika video zao.
Hiyo ilitosha kunifanya mimi nikuone kwamba unahitaji kubadilika. Unahitaji kutafuta kazi ya kufanya kuliko kuishi kimjinimjini. Mbona unaonekana unaweza hata kuigiza, kwa nini usiigize? Unafikiri aina ya maisha unayokwenda nayo itadumu hadi lini?
Mimi nakushauri kama kaka yako, badilika. Wenzako pia wenye kamchezo kama ka kwako nao pia nawaambia wabadilike ili na wao wafanye kazi, waache kuweka picha za nusu utupu mitandaoni.
Ni matumaini yangu wewe pamoja na wenzako wote wanaofanya mambo hayo watabadilika mara moja maana si ungwana.
Mimi kaka’ko;
Erick Evarist
Chanzo:GPL
0 Response to "Masogange na Wenzako Tumieni Ujana Wenu Vizuri"